Wananchi wa Wilaya ya Hanang’ watanufaika na mradi mkubwa wa maji wenye thamani ya shilingi bilioni 3.6, unaolenga kurejesha miundombinu ya maji katika vijiji vya Kata ya Gendabi na Kata ya Mogitu . Maeneo haya yaliathirika vibaya kutokana na maporomoko ya tope na mawe yaliyotokea Desemba 2023, na kusababisha uharibifu wa vyanzo vya maji, vituo vya maji, na vinywesheo vya mifugo.
Katika hafla ya utiaji saini wa mkataba wa ujenzi wa mradi huo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Cuthbert Sendiga, aliwataka wakandarasi kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati kama ilivyoainishwa kwenye mkataba, akisisitiza kuwa hakuna nafasi ya ucheleweshaji, kwani wananchi wanahitaji huduma hiyo haraka ili kurejesha hali ya kawaida katika maisha yao.
“Serikali inajali ustawi wa wananchi wake, na ndio maana tumeweka kipaumbele katika kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati. Nataka niwaonye wakandarasi kuwa hatutakubali visingizio vyovyote vya kuchelewesha mradi huu. Wananchi wanahitaji maji, na ni wajibu wetu kuhakikisha wanayapata,” alisema Mhe. Sendiga.
Kwa upande wake, Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Manyara, Mhandisi James Kionaumela, alieleza kuwa athari za maporomoko ya tope zilikuwa kubwa sana, huku bwawa lililotumiwa na wakazi wa Kitongoji cha Gaulol/Basodagwargwe likiwa limechafuliwa na tope na kuwa si salama kwa matumizi.
“Kwa sasa wakazi wapatao 75,166 wa maeneo haya hawana huduma ya maji safi na salama. Mradi huu utahakikisha miundombinu ya maji inarejeshwa, na tunatekeleza hatua za dharura, muda mfupi na muda wa kati ili kuhakikisha wananchi wanapata maji haraka,” alisema Mhandisi Kionaumela.
Mhandisi Kionaumela amesema itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa viwango vya juu na kukamilika ndani ya muda uliopangwa. Wananchi pia wanahimizwa kushirikiana na viongozi wa mradi huo ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kwa ufanisi na bila changamoto zisizo za lazima.
Mradi huu ni moja ya jitihada za serikali katika kuboresha huduma ya maji vijijini, ili kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma hiyo kwa urahisi na kwa gharama nafuu.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.