Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.3 kwa vikundi 92 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia mpango wa asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili kwa wanufaika wa awamu ya pili ya mikopo hiyo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wilaya ya Hanang’, William Gaudence, alisema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwawezesha kiuchumi Watanzania wote, hususan makundi yenye uhitaji maalum.
“Halmashauri ilianza kwa kutoa milioni 504 kwa vikundi 33 katika awamu ya kwanza, na sasa tumewafikia vikundi 59 kwa mkopo wa milioni 799. Tukijumlisha awamu ya kwanza na ya pili, Halmashauri ya Wilaya ya Hanang sasa itakuwa imetoa zaidi ya shilingi bilioni moja na mia tatu” alisema Gaudence na kuongeza kuwa mafanikio ya wanufaika yatafungua fursa zaidi kwa wengine.
Vikundi hivyo 59 vilivyopata mafunzo katika ukumbi wa Shule ya Msingi Katesh A, vinajumuisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu waliopatiwa elimu ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha, mbinu za urejeshaji wa mikopo, pamoja na maadili ya uongozi wa vikundi.
Kati ya shilingi milioni 799 zilizotolewa, vikundi 31 vya wanawake vimepata milioni 486.9, vijana milioni 282.5, na vikundi vinne vya watu wenye ulemavu milioni 29.6.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Hanang’, Mwalimu Athuman Likeyekeye, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya, aliwataka wanavikundi kutumia fedha walizopokea kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha wanarejesha mikopo kwa wakati.
“Tunaamini fedha hizi zikitumika vizuri zitaenda kuongeza uchumi kwa Wanahang na hili ni deni la heshima. Wenzenu wanawasubiri. Urejeshaji wa mikopo hii ndio utakaofanikisha mzunguko wa maendeleo katika jamii yetu,” alisema Likeyekeye.
Halmashauri imeahidi kuendelea kutoa mafunzo na usaidizi wa kitaalamu ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo endelevu na halisi kwa familia na jamii kwa ujumla.
Katika wakati ambapo juhudi za kukuza uchumi wa ndani zinazidi kupewa kipaumbele, mfano wa Hanang’ unaweza kuwa dira kwa halmashauri, ikionyesha kuwa uwekezaji kwa watu ni chachu ya mabadiliko ya kweli.
Hanang' District Council Headquater located at the Northern part of Katesh town in Ganana Ward
Postal Address: P.O Box 02 Katesh-Hanang'
Telephone: 027-2530022 / 42
Mobile: +255 762 362 950
Email: ded@hanangdc.go.tz
Copyright ©2016 GWF . All rights reserved.